Tuesday, 4 August 2015

MANDAGO AWATAKA VIONGOZI KUWA WAVUMILIVU



Gavana wa kaunti ya Uasin Gishu Jackson Mandago, amewataka viongozi wote nchini kuweka tofauti zao za kisiasa kando, ili kuunga mkono sera za serikali kuu iwapo wanataka maendeleo mashinani. Mandago amesema kuwa serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu inaunga serikali kuu mkono kwa kila jitihada inazochukua kufanya maendeleo.

Akizungumza na wanahabari afisini mwake  gavana huyo amesema kuwa shida zinazowakumba wakaazi wa kaunti ya Uasin Gishu na Kenya kwa jumla zitakabiliwa tu iwapo viongozi watakuwa tayari kufanya kazi kwa pamoja.

Aidha Mandago amewataka viongozi wote nchini kuwa wavumilivu na kufanya mazungumzo katika kushughulikia shida zinazozikumba serikali za kaunti.

Thursday, 16 July 2015

HOSPITALI YA WEBUYE KUKARABATIWA



     Usimamizi wa hospitali ya wilaya ya Webuye utaanzisha shughuli za kurekebisha vyumba vya kuwazalishia akina mama wajawazito hivi karibuni.
     Wakiongozwa na daktari mkuu katika hospitali hiyo Isaac Omeri, viongozi hao wamesema kuwa wana nia ya kuinua sekta ya uzalishaji wa akina mama, ili huduma katika sekta hiyo iimarike zaidi.
     Awali, hospitali ya Webuye ilituzwa kama hospitali bora nchini mwaka wa elfu mbili na kumi na mbili katika huduma za uzalishaji wa akina mama, katika zoezi hilo lililojumuisha hospitali zote za viwango vya nne nchini. Sasa viongozi kwenye hospitali hiyo wanatarajia tuzo zaidi kufuatia ukarabati huo.
     Haya yanajiri huku ukarabati wa vyumba vya kuhifadhi maiti ukiendelea kwenye hospitali hiyo ya Webuye.

ASANTE LUSAKA - DAKTARI



     Mkuu wa madaktari kwenye hospitali ya wilaya mjini Webuye, amempongeza gavana wa kaunti ya Bungoma Kenneth Lusaka kwa juhudi zake za kuinua viwango vya afya kwenye kaunti hiyo.
     Akizungumza afisini mwake mapema hii leo, daktari Isaac Omeri amesema kuwa serikali ya kaunti imetia fora kuona kuwa afya inapewa kipaumbele, na akamuomba gavana Lusaka kuendeleza juhudi hizo.
     Hata hivyo, Omeri amesema kuwa fedha zinazopeanwa kwa sekta ya afya katika kaunti hiyo ni chache, na kuwa haziwezi kuiendesha sekta hiyo kikamilifu huku akisema kuwa hospitali hiyo imekuwa ikitegemea pesa zinazokusanywa kutoka kwa wagonjwa ambazo pia hazitoshi.
     Vilevile daktari huyo ameomba uongozi wa kaunti hiyo ya Bungoma kutafuta mbinu mbadala za kupata fedha, na kutotegemea serikali ya kitaifa ili kukuza sekta muhimu kwenye kaunti hiyo.

Wednesday, 15 July 2015

WEBUYE - DEREVA MAHAKAMANI KUHUSU AJALI YA KIPKAREN



     Dereva wa matatu iliyohusika kwenye ajali ya barabara na kusababisha vifo vya watu tisa eneo la Kipkaren mwezi mmoja uliopita ametozwa faini ya shilingi elfu thelathini pesa taslimu na mahakama ya Webuye.



     Akitoa umamuzi huo hakimu mkaazi wa Webuye Stella Nabwire amesema kuwa mshukiwa huyo kwa jina Vincent Matayo amekiri madai ya kuendesha gari kwa kasi na kukiuka sheria za barabara huku akionywa dhidi ya kurudia kosa hilo na kuwa atapokonywa leseni hiyo ikiwa atahusika kwenye ajali nyingine chini ya miezi sita ijayo.
  
   Nabwire ameitaka mamlaka ya kitaifa ya uchukuzi NTSA kushirikiana na idara ya trafiki kuwahamasisha madereva na wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za trafiki ili kupunguza visa vya ajali za barabarani.

KAUNTI YA BUNGOMA - USALAMA WAIMARISHWA KATA NDOGO YA MATULO




     Usalama umeimarishwa katika eneo la Matulo kijiji cha Weighbridge kata ndogo ya Matulo kufuatia visa vya ukosefu wa usalama ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa siku za hivi majuzi.

     Mwenyekiti wa mpango wa nyumba kumi katika eneo hilo Thomas Abukuse amesema kuwa, wamekuwa wakitoa taarifa muhimu zinazohusiana na usalama kwa maafisa wa polisi, hatua ambayo imepelekea kuimarika kwa hali ya usalama, huku akitoa wito kwa kwa wadau katika sekta ya usalama kushirikiana zaidi  ili kuwarahisishia majukumu yao.

     Ni mpango ulioanzishwa na serikali ya kitaifa yapata miaka miwili iliyopita, lengo kuu likuwa ni kuimarisha usalama.